TFNC yatoa semina ya ulaji unaofaa TAWLA kupitia mkutano mtandao

News Image

Imewekwa: 20th May, 2025

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imetoa semina ya ulaji na mitindo bora ya maisha ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa wafanyakazi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA).

Akitoa semina hiyo kupitia mkutano mtandao (zoom meeting), Afisa Lishe Mwandamini kutoka TFNC, Adeline Munuo amesema kuwa lengo la semina hiyo ni kuwawezesha watumishi wa TAWLA kuelewa na kuzingatia ulaji bora na mtindo mzuri wa maisha ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

“Kupitia semina hii, tumeweza kuwaeleza wafanyakazi wa TAWLA dhana ya magonjwa yasiyombukiza, tabia hatarishi zinazochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo na namna ya kujikinga kupitia ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha” amesema Munuo.

Munuo ametaja njia mbalimbali za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo; kutumia vyakula vya asili zaidi kama vile nafaka zisizokobolewa, kula mbogamboga na matunda kila siku angalau aina tano, kupunguza vyakula vilivyosindikwa (high processed foods) kama vile soseji, biskuti na vinjwaji vyenye sukari. Njia nyingine alizozitaja ni kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari, mafuta na chumvi kwa wingi pamoja na kufuatilia uzito na mzunguko wa kiuno mara kwa mara.

Aidha Munuo amesema kuwa ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha ni kinga bora ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, maonjwa ya moyo na baadhi ya saratani ambayo yamekuwa na gharama kubwa katika kuyatibu, na kudhohofisha nguvu kazi. Hivyo ametoa wito kwa taasisi mbalimbali kujiwekea utaratibu wa kuwapia semina za namna hiyo watumishi wake kwani ili kuimarisha afya zao na kuwa na uhakika wa nguvu kazi yenye tija.

Kwa upande wake Afisa Sheria wa TAWLA, Yosia Kimweri ameishukuru TFNC kwa kuwapatia semina hiyo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa rasilimali yenye tija na endelevu katika kufikia malengo ya taasisi yao.

“Sasa hivi kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanachangia kufifisha uwezo wa nguvu kazi kufanya kazi kwa tija. Hivyo kupitia semina hii tuliyopewa na wataalamu kutoka TFNC tunaamini kuwa itatusaidia mtu mmoja mmoja na Taasisi kwa ujumla kuwa na wafanyakazi wenye afya njema” Amsema Kimweri