Awali wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Dkt. Esther Nkuba amesema kuwa wauguzi na wakunga ni watu muhimu sana katika kufanikisha suala la unyonyeshaji katika jamii.
“Takwimu za mwaka 2022 za TDHS zinatuonesha kuwa watoto wanaoanzishiwa kunyonyesha maziwa ya mama ndani ya saa moja ni baada ya kuzaliwa ni asilimia 70, na watoto wanaopewa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ni asilimia 64, lengo letu ni kufika asilimia 100, na hili linawezekana ndio maana tumeanza kutoa mafunzo haya kwa wauguzi na wakunga kwa sababu ni watu muhimu sana katika kufanikisha unyonyeshaji katika jamii” Amesema Dkt. Nkuba.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo Eliasaph Mwana amesema kuwa kozi hii imetolewa kwa siku nne kuanzia tarehe 23/05/2023 hadi tarehe 26/05/2023 ambapo jumla ya watu watano waliweza kushiriki na kuhitimu mafunzo hayo.
“Jumla ya watu 30 walifanya maombi ya kusoma kozi hii lakini walioweza kujiunga na kuhudhuria ni watu watano tu, hivyo tutafanya tathimini kubaini ni changamoto gani zilizosababisha watu wengi kushidwa kuhudhuria ili tutakapotangaza tena kozi hii watu wengi waweze kuhudhuria” amesema Mwana.
Naye Mkunga kutoa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga ambaye amehudhuria mafunzo hayo ametoa rai kwa TFNC kuangalia ni kwa namna gani wataweza kutoa mafunzo haya mikoani ili kuhakikisha elimu hii inawafikia watu wengi zaidi.
|