TFNC YAJIPANGA KUTANUA WIGO WA KUFIKISHA ELIMU SAHIHI YA LISHE KWA WATANZANIA
20 Aug, 2026
TFNC YAJIPANGA KUTANUA WIGO WA KUFIKISHA ELIMU SAHIHI YA LISHE KWA WATANZANIA
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imejipanga kuendelea kupanua wigo wa utoaji wa elimu sahihi na yenye ushahidi kuhusu lishe kwa watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.   Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa TFNC, Bw. Hamza Mwangomale, wakati akiwasilisha mipango na mikakati ya kitengo hicho katika kufikisha elimu ya lishe kwa umma, wakati wa ziara rasmi ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dkt. Germana Leyna, pamoja na Timu ya Menejimenti ya Taasisi.   Akiongea wakati wa ziara hiyo, Dkt. Leyna amesema kuwa uhitaji wa elimu sahihi ya lishe nchini unaendelea kuongezeka siku hadi siku, huku teknolojia ya mawasiliano ikiendelea kuwa nguzo muhimu. Hivyo ametoa rai kwa kitengo cha Mawasiliano TFNC kuongeza ubunifu katika kufikisha elimu ya lishe kwa umma, ili kuhakikisha kila mtanzania anapata taarifa sahihi za lishe.                   Kwa upande wake Bw. Mwangomale ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, TFNC kupitia kitengo cha mawasiliano inalenga kuwafikia Watanzania zaidi ya milioni 12 kupitia vipindi vya runinga, redio na mitandao ya kijamii vitakavyolenga kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia katika ulaji na mitindo bora ya maisha   Aidha, Bw. Mwangomale amesema kuwa TFNC inalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kwa kuwapatia mafunzo na nyenzo sahihi za utoaji wa taarifa sahihi za lishe, ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa lishe kupitia vyombo vyao vya habari na kusaidia kupunguza usambazaji wa taarifa zisizo sahihi kuhusu lishe.    "Sekta ya afya na lishe inakabiliwa kwa kiwango kikubwa na usambaaji wa taarifa potofu hususani katika mitandao ya kijamii. Hivyo kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuripoti kwa usahihi taarifa za lishe itasaidia kufikisha elimu hiyo kwa watu wengi zaidi" Amesema Mwangomale.