20 Aug, 2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna, na timu ya Menejimenti ya Taasisi, imekutana na watumishi wa Idara ya Sayansi ya Chakula na Lishe (FSN) iliyopo Mikocheni Dar es Salaam katika ziara ya kutembelea Idara, Sehemu na Vitengo vya Taasisi kwa lengo la kupitia mafanikio ya utekelezaji wa kazi za mwaka 2025/2026 na mikakati waliyojiwekea kwa mwaka 2026/2027
Akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya Idara, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Chakula na Lishe, Tedson Lukindo ameeleza kuwa Idara yake imejipanga kuhakikisha TFNC inaendelea kuwa kinara katika kufanya uchunguzi na uchambuzi wa kitaalamu wa bidhaa za chakula, pamoja na kuchangia katika uendelezaji na uzalishaji wa bidhaa bora za lishe.
"Idara inatekeleza majukumu mbalimbali yanayochangia katika kukabilina na matatizo ya utapiamlo nchini, katika mwaka wa fedha 2026/27 Idara imejipanga kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa bora za lishe kwa kufanya uchambuzi wa kimaabara wa kubaini wingi wa virutubishi katika sampuli za vyakula na kutoa mafunzo kwa wasindikaji wa chakula cha watoto wenye umri wa miezi sita na kuendelea kwa kutumia unga mchanganyiko" amesema Lukindo.
Aidha, katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana, mipango ya idara pamoja na changamoto mbalimbali za kiutendaji zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ambazo zote zilitolewa ufafanuzi na maelekezo ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Ziara hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na timu ya Menejimenti katika idara mbalimbali za Taasisi inaendelea na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 21 Agosti 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mawasiliano na watumishi, kufuatilia utekelezaji wa majukumu na kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji wa TFNC.
