TFNC YAHIMIZWA KUONGEZA KASI KUPATA ITHIBATI YA KIMATAIFA (ISO)
22 May, 2026
TFNC YAHIMIZWA KUONGEZA KASI KUPATA ITHIBATI YA KIMATAIFA (ISO)
Serikali imeitaka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kuharakisha mchakato wa kupata ithibati ya kimataifa (International Accreditation) kwa ajili ya maabara yake ya Chakula na Lishe iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Hatua hiyo inatajwa kuwa itafanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za chakula na lishe zinazokidhi viwango vya kidunia, huku ikifungua milango mipana ya masoko na ushirikiano wa kimataifa. Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uchunguzi na Matengenezo ya Vifaa Tiba, Dkt. Alex Magesa, akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati wa kuhitimisha mafunzo maalumu ya Usalama wa Maabara na Mipango ya Hatua za Kupata Ithibati (Laboratory Safety and Accreditation Road Map Training) yaliyoandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa watalaamu wake wa Maabara na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mkoani Kilimanjaro. “Dhamira ya Serikali ni kuona maabara zetu zote, ikiwemo ya TFNC, zinafikia viwango vya ISO ili majibu yanayotoka yaweze kuheshimika na kukubalika popote duniani,” amesema Dkt. Alex. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuiandaa maabara hiyo iliyopo kufikia viwango vya juu vya ubora. “kupata ithibati ya kimataifa (ISO) siyo tu kutaongeza uaminifu wa majibu ya sampuli za chakula na lishe zinazopimwa nchini, bali pia kutahakikisha usalama wa wataalamu wanapokuwa kazini na kuisaidia taasisi hiyo kutoa huduma zinazokubalika katika soko la kimataifa” amesema Dkt .Germana.   Pia Wataalamu wetu wa Maabara wamefanikiwa kuhitimu mafunzo maalumu ya Usalama wa Maabara na Mipango ya Kupata Ithibati (Laboratory Safety and Accreditation Road Map). Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wetu wa kuhakikisha huduma za uchunguzi wa chakula nchini zinafikia viwango vya juu vya ubora wa kimataifa.  Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ni maabara rejea kwenye ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kati na Kusini, na matokeo ya uchunguzi wa vya hali ya lishe na virutubishi yanayotolewa na maabara hii, yanaaminika kimataifa (WHO, CDC, ECSA-HS, IGAD), na kuifanya kuwa maabara pekee ya lishe inayoaminika ukanda huu.