22 May, 2026
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa lishe, imeanza mchakato wa awali wa kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa takwimu za matumizi ya chumvi yenye madini joto nchini, hatua inayolenga kuimarisha udhibiti na ufuatiliaji wa hali ya madini joto katika jamii.
Mchakato huo umeanza kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali mkoani Morogorokujadili namna bora ya kukusanya na kuchambua takwimu kupitia sampuli za chumvi kutoka ngazi ya jamii pamoja na sampuli za mikojo kutoka kwa wajawazito wenye umri wa miaka 15 hadi 49 walio katika hatua za awali za ujauzito chini ya wiki 12.
Aidha TFNC imetumia kikao hicho, kuwasilisha na kujadili matokeo ya Utafiti wa Mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za matumizi ya Chumvi yenye madini joto (FORTIMAS), ambao ulianza kutekelezwa katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Singida na Mtwara na baadae kuongezeka kwa mikoa ya Simiyu na Manyara , huku utafiti huu pia unatarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar ukiendelea kutekelezwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Zanzibar, Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Iodine Global Network kupitia ufadhili wa UNICEF.
Matokeo ya utafiti wa FORTIMAS yatasaidia kuongeza mbinu za kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na upatikanaji wa taarifa za chumvi yenye madini joto ngazi ya kaya kwa wakati na urahisi zaidi na kupata takwimu muhimu kwa ajili ya kuona mwenendo wa tatizo la Upungufu wa madini joto nchini.
