TFNC, Wizara ya Elimu kuzindua Mwongozo wa Utoaji wa huduma ya Chakula na Lishe shuleni Oktoba 29

News Image

Imewekwa: 27th Oct, 2021

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna amesema kuwa Taasisi inatarajia kushiriki katika uzinduzi wa Mwongozo wa utoaji wa Huduma ya Chakula shuleni tarehe 29 Oktoba, 2021 jijini Dodoma. Dkt. Leyna amebainisha hilo wakati akitoa salamu za Taasisi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa iliyofanyika tarehe 23 Oktoba, 2021 mkoani Tabora.

“kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzinduliwa rasmi kwa maadhimisho haya tarehe 7 Agosti 2020 jijini Dodoma, Taasisi imepata mafanikio mengi, na moja ya mafanikio hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tumeweza kuandaa mwongozo wa utoaji wa chakula shuleni” amesema Dkt. Leyna.

Dkt. Leyna amesema kuwa mwongozo huu utaziwezesha shule za msingi na sekondari kuwa na utaratibu maalum wa huduma ya chakula utakaowezesha kupata chakula bora kitakachotosheleza mahitaji ya ki-lishe kwa wanafunzi na hivyo kuwawezesha kuepukana na matatizo ya lishe duni au lishe iliyozidi.

“lishe bora kwa wanafunzi huwawezesha kuwa wabunifu darasani, kufaulu vizuri na baadae kuendesha gurudumu la Serikali na kuwezesha nchi kuwa nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati”amesema Dkt. Leyna