TFNC, PANITA wawajengea uwezo waandishi wa habari

Imewekwa: 6th Jun, 2025
Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) wamendesha semina ya siku moja kwa waandishi wa habari nchini inayolenga kuongeza uelewa wao juu ya mambo mbalimbali ya lishe ikiwemo michakato ya “Nutritionfor Growth”, hali ya lishe nchini, mipango ya sasa ya Serikali, na jukumu la vyombo vya habari katika kuboresha lishe na kuongeza uelewa wa umma juu ya masuala ya lishe.
Akiongea wakati wa kufua semina hiyo Mkurugenzi wa PANITA, Tumaini Mikindo amesema kuwa waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika kuufikia umma.
“Masuala ya lishe ni mtambuka, yanahitaji jitihada ya sekta mbalimbali ndio maana zamani wakati suala hili lilihusisha sekta ya afya pekee matatizo ya lishe yalikuwa yanadhibitiwa na kujirudia mara kwa mara, mfano mkoa wa Iringa katika miaka ya tisini, Serikali ilitangaza kutokomeza kabisa tatizo la udumavu, lakini baada ya muda tatizo hilo lilibuka tena kwa kasi kubwa. Hivyo tunatamani kuona kila mmoja anashiriki katika mapambano dhidi ya aina zote ya utapiamlo, na kama vyombo vya habari vitasemea kwa usahihi taarifa za lishe, jambo hili litawezekana. ” Amesema Mikindo.
Akiwasilisha mada wakati wa semina hiyo, Afisa Mtafiti wa Sera na Mipango ya Lishe kutoka TFNC, Geofrey Chiduo amesema kuwa sasa Tanzania kumekuwa na ongezeko kubwa la kusambaa taarifa zisizo sahihi za masuala ya lishe, huku waandishi wa habari wakiwa ni sehemu moja wapo ya kusambaza taarifa hizo, jambo linalotishia usalama wa afya na lishe ya jamii.
Chiduo amesema kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo kwani mtu akiwa na lishe bora afya yake huimarika na hivyo kuweza kufanya kazi kwa tija. Hivyo ametoa rai kwa waandishi wa habari nchini kuhakikisha wanaongeza umakini na kuzuia upotoshaji wa taarifa za lishe.
“Ni vyema mwandishi wa habari wakawa na uelewa sahihi wa jambo analoripoti ili kuzuia upotoshaji pale unapotokea. Mfano kunachombo kimoja sitakitaja jina lakini walikuwa wanamuhoji msanii wa kike ambaye alikuwa anajisifu kwamba amemnyonyesha mwanaye kwa muda wa wiki mbili tu na kumuachisha ziwa, na mtoto wake hajapata matatizo yoyote ya kiafya. Mtangazaji aliyekuwa anafanya mahojiano hayo kama angekuwa na uelewa sahihi wa masuala ya lishe, basi angemrekebisha msanii huyo, na hivyo mtazamaji angepata ujumbe sahihi yuu ya umuhimu wa kumnyonyesha mtoto na faida ya maziwa ya mama kiafya” Amesema Chiduo.
Akitoa neno la shukrani kwa PANITA na TFNC kutoa semina hiyo kwa waandishi wa habari, Mhariri wa Press Media, Neville Meena amesema kuwa mafunzo waliyoyapata katika semina hiyo yamewajenga sana wao binafsi kama waandishi wa habari kwa kutambua umuhimu wa lishe katika maisha ya kila siku. Pia amesema kuwa hii itasaidia kuongeza hari za waandishi wa habari kuripoti zaidi taarifa za lishe kwani kwa sasa masula ya lishe hayapewi sana kipaumbele katika vyombo vingi vya habari.
“Tunaomba PANITA na TFNC waendelee kutupatia mafunzo ya namna hii mara kwa mara kwani itasaidia kutufanya kuwa wabobezi katika kuandika na kuripoti taarifa za lishe, kwa mfano tunaenda bungeni kuripoti bajeti za wizara mbalimbali. Hivyo kupitia mafunzo haya sisi kama waandishi wa habari tunaweza kujiuliza ni kwa namna gani bajeti hizo zimegusia masuala ya lishe, ikizingatiwa kuwa lishe ni sekta mtambuka” amesema Meena.