TFNC na WFP yazidi kuwafikia wanafunzi wasioona kwenye elimu ya masuala ya chakula na lishe

News Image

Imewekwa: 21st Apr, 2024

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limefanikiwa kuwafikia wanafunzi wasioona wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe na Shule ya Msingi Irente iliyopo Wilayani Lushoto Mkoani Tanga kwa kuwakabidhi vitabu vya Maandishi yanukta nundu na Redio zenye ujumbe muhimu wa lishe ili kuwawezesha kupata elimu ya masuala ya Chakula na lishe ambayo awali ilikuwa changamoto kwao kuipata kutokana na aina ya ulemavu waliokuwa nao.

Nyenzo hizo muhimu kwa watu wasioona zimekabidhiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB) Bwa. Omary Itambu, ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kuwafikishia wanafunzi wasioona ujumbe muhimu wa lishe kupitia Maandishi ya nukta nundu na sauti, ili kuwawezesha nao kuendelea kupata elimu ya lishe kama ilivyo kwa wanafunzi wengine wenye uwezo wa kuona.

Bw. Omary amesema lishe ni suala mtambuka na muhimu kwa vijana waliopo shuleni kuweza kulifahamumapema wakiwa bado wadogo, hivyo TAB kwa kushirikiana na TFNC pamoja na WFP imeona ni muhimu kuhakikisha makundi yote yanafikiwa na elimu hiyo ikiwemo watu wasioona.

Jumla ya Vitabu 100 vyenye Maandishi ya Nukta nundu na Redio za 100 zenye ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona, zimetolewa kwa mkoa wa Tanga na kukabidhiwa kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Shule ya Msingi Irente Lushoto, na Shule ya Msingi Pongwe iliyopo Jiji la Tanga. Nyenzo hizo zitatumiwa na wanafunzi wasioona shuleni humo,kwaajili ya kupata elimu ya masuala ya chakula na lishe.