TFNC NA WFP yawafikia watu wasioona kwenye utoaji elimu ya lishe

Imewekwa: 21st Mar, 2023
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia Ufadhili wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imewafikia watu wasioona, mara baada ya kuzindua nyenzo zenye ujumbe wa lishe kwa kundi hilo, ambazo zimeandaliwa katika maandishi ya nukta nundu na nyingine kwenye mfumo wa sauti. Hafla fupi ya uzinduzi huo imefanyika Machi 21, 2023, katika Ofisi za Taasisi ya Chakula jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa lishe akiwemo Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bi. Sarah Gordon-Gibson. |
![]() |
Akizundua kitabu cha ujumbe huo wa lishe kwa jamii ya watu wasioona, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Esther Nkuba amesema kitabu hicho kinalenga kuelimisha na kuhamasisha jamii ya watu wasioona kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa ustawi, ukuaji na maendeleo ya watoto na afya ya watu wa jamii hiyo kwa ujumla. Dkt.Nkuba amesema Taasisi imeyafikia makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo wanawake wajawazito, wanaonyonyesha, watoto wadogo na wachanga, vijana balehe, na wazee, huku kundi la wasioona likisahulika, hivyo ujio wa nyenzo hii utawasaidia nao kuweza kufikiwa na elimu ya lishe ambayo Taasisi imekuwa ikiitoa. Kwa Upande wake mwakilishi mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Bi. Sarah Gordon-Gibson amesema waliamua kuunganisha nguvu na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ili kuweza kuandaliwa kwa nyezo hizo zenye ujumbe wa lishe kwa watu wasioona, mara baada ya kugundua jamii hiyo inakosa fursa ya kupata elimu sahihi kuhusu masuala ya chakula na lishe. “Watu wenye matatizo ya kuona hawawezi kupata taarifa za lishe kupitia vyombo vya habari vya magazeti, kama vile mabango na vipeperushi. Kwa hivyo, ilikuwa ni lazima kuendeleza afua zinazofaa na zilizolengwa ili kuwahimiza kufuata tabia na mitindo ya maisha chanya ya lishe.” Alisema Bi.Gordon. |