TFNC na WFP yagawa vitabu vya braille na radio zenye ujumbe wa lishe kwa watu wasioona

Imewekwa: 24th Feb, 2024
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imekabidhi vitabu 170 kati ya 500 vyenye ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona vilivyoandaliwa kwa maandishi ya nukta nundu (Braille) pamoja na redio 50 kati ya 500 zilizorekodiwa ujumbe huo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Braille Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida tarehe 22 Februari, 2023.
Nyenzo hizo muhimu kwa watu wasioona zimekabidhiwa kwa Mgeni Rasmi wa Kilele cha Maadhimisho hayo Dkt. Wilson Mahera Charles ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe, ambaye alimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB)
Awali akitoa salamu za TFNC, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe Dkt. Esther Nkuba amesema, jamii ya watu wasioona inakabiliwa na changamoto ya kupata taarifa na elimu sahihi ya masuala ya afya na lishe na sababu kubwa ikiwa ni kutokana na aina ya ulemavu walionao.
Dkt. Nkuba amesema changamoto hiyo iliisukuma Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kutengeneza vitabu 500 vya Braille na Radio 500 zenye masomo ya Lishe ili kumuwezesha mtu asiyeona kupata elimu sahihi ya lishe.
Aidha Dkt. Nkuba amesema katika awamu ya kwanza Taasisi inakabidhi vitabu 170 na radio 50 ambazo zitakabidhiwa kwa maafisa elimu wa mikoa sita ya Singida, Dodoma, Tabora, Njombe, Mwanza na Shinyanga na vilivyobakia vitakabidhiwa kwa Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB) kwa ajili ya kugawa maeneo mengine yenye uhitaji.
Naibu Katibu Mkuu,OR-TAMISEMI anayeshughulika na Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe, Dkt. Wilson Mahera Charles akikabidhi vitabu vya nukta nundu (Braille) na redio zenye ujumbe wa lishe kwa Maafisa Elimu Maalumu wa mikoa ya Singida, Dodoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Njombe kwa ajili ya kuvisambaza katika shule zenye wanafunzi wasioona wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Braille Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida tarehe 22/02/2024.