TFNC na Iodine Global Network(IGN) kufanya utafiti wa mfumo wa ufuatiliaji wa takwimu za chumvi yenye madini joto

News Image

Imewekwa: 20th Sep, 2024

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Iodine Global Network (IGN) wanatarajia kufanya Utafiti wa majaribio ya Mfumo wa ufuatiliaji wa Takwimu za Chumvi utakaojulikana kama FORTIMAS, lengo likiwa kutafuta njia nyepesi na endelevu ya kupata takwimu muhimu kwa ajili ya kuona mwenendo wa tatizo la Upungufu wa madini joto nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amesema Utafiti huo utafanyika katika Mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Singida na Mtwara na amesema utafiti huo utaenda kutafuta njia endelevu na yenye gharama nafuu ya kuweza kutathmini upatikanaji wa madini joto katika kaya na jamii kwa ujumla.

“Kwa miaka mingi sana taifa letu limekuwa likitegemea Utafiti ya Afya na Mama na mtoto (TDHS) katika kuweza kupata taarifa za upatikanaji wa chumvi yenye madini joto katika jamii yetu hivyo tumeona kuna haja ya kuja na njia nyingine rafiki na rahisi yenye gharama nafuu ambayo itaweza kutupa pia taarifa zinazohusiana na madini joto wa urahisi na zenye usahihi”. Amesema Dkt. Germana Leyna.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Iodine Global Network kwa ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika Prof. Festo Kavishe, amesema Tanzania imechaguliwa kufanya utafiti huu kutokana nakupiga hatua kubwa katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa madini joto kwa watu wake.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Afisa Lishe lishe wa mkoa huo Bi. Mwanamvua Zuberi, amesema wao kama mkoa watashiriki kikamilifu katika kuhakikisha utafiti huu unafanyika kwa ufanisi, kwani takwimu sahihi zitakazopatikana zitasaidia nchi kukabiliana na tatizo la upungufu wa madini joto .