TFNC kuja na mpango wa utoaji mafunzo ya ulishaji wa watoto kwa njia ya mtandao (E- Learning)

Imewekwa: 9th Aug, 2021
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Germana Leyna amesema kuwa TFNC ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mafunzo ya ulishaji wa watoto wachanga na wadogo kwa njia ya mtandao (E- Learning) yatakayotolewa kwa watoa huduma za afya na wananchi kwa ujumla. Dkt. Leyna ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani 2021 yaliyofunguliwa kitaifa tarehe 01/08/2021 na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mhe. Cosmas Nshenye katika viwanja vya Vwawa CCM wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.
Dkt. Leyna amesema kuwa mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika kukabiliana na udumavu wa watoto kwa sababu yatawafikia watu wengi zaidi.
“Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni nyenzo muhimu katikakukabiliana na aina zote za utapiamlo (lishe pungufu nailiyozidi) kwa watoto kwa sababu huleta uhakika waupatikanaji wa chakula kwa watoto wachanga na wadogokwa usahihi.” Amesema Dkt. Leyna
Pia Dkt. Leyna amesema kuwa mafunzo hayo yatawapatia stadi muhimu kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakumba akina mama wanaonyonyesha na kusababisha kutofuata taratibu sahihi za ulishaji na unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Aidha Dkt. Leyna ametoa wito kwa wananchi kufuata kanuni sahihi za unyonyeshaji ambazo ni pamoja na; kunyonyesha ndani ya saa moja baada ya mtoto kuzaliwa, watoto kunyonyeshwa maziwa ya mwanzo yenye rangi ya njano, watoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi 6 ya mwanzo, watoto kuanzishiwa chakula cha nyongeza baada ya kufikisha miezi sita na kuendelea kunyonyeshwa mara kwa mara kadri anavyohitaji hadi anapofikisha umri wa miaka miwili.