03 Sep, 2026
DAR ES SALAAM: Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imejipanga kuimarisha uchunguzi na uchambuzi wa kitaalamu wa bidhaa za chakula, pamoja na kuongeza ufanisi katika uendelezaji na uzalishaji wa bidhaa bora za lishe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto za utapiamlo nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Chakula na Lishe (FSN), Tedson Lukindo, wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dkt. Germana Leyna, pamoja na timu ya Menejimenti katika idara, sehemu na vitengo mbalimbali vya Taasisi, iliyofanyika katika Ofisi za Idara hiyo zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam.
Ziara hiyo imelenga kupitia utekelezaji wa majukumu na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/2026, pamoja na kujadili mikakati na mipango ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo, Lukindo alisema kuwa FSN imejiwekea mikakati ya kuhakikisha TFNC inaendelea kuwa kinara katika kufanya uchunguzi na uchambuzi wa kitaalamu wa bidhaa za chakula, pamoja na kuchangia katika uendelezaji na uzalishaji wa bidhaa bora za lishe.
Aidha, alisema kuwa kupitia utekelezaji wa mipango hiyo, Idara inalenga kuendelea kutoa mchango katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa salama, bora na zenye virutubishi vinavyokidhi mahitaji ya lishe ya wananchi, hususan watoto.
Katika kikao hicho, watumishi wa Idara walipata fursa ya kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana, mipango ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, pamoja na changamoto mbalimbali za kiutendaji zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.
Changamoto hizo zilipatiwa ufafanuzi na maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji na timu ya Menejimenti, kwa lengo la kuwezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kufikia malengo yaliyowekwa na Taasisi.
Ziara hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC pamoja na timu ya Menejimenti katika idara, sehemu na vitengo mbalimbali vya Taasisi ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mawasiliano ya ndani, kusikiliza na kutatua changamoto za kiutendaji, kufuatilia utekelezaji wa majukumu na kuweka mikakati ya kuimarisha ufanisi katika utendaji wa TFNC.
