Makatibu wakuu kutoka katika sekta mtambuka nchini wamepongeza hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Lishe wa Muda Mrefu, huku wakiahidi kutoa ushirikiano kupitia sekta zao ili kusaidia kukamilika kwa wakati na kupata msukumo katika utekelezaji ili kuboresha hali za lishe za watanzania
Hayo yamejiri katika kikao maalumu cha kusimamia na kushauri utekelezaji wa masuala ya Lishe nchini kilichofanyika tarehe 18/9/2026 katika ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam ambacho kimeongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mheshimiwa Dkt. Jim Yonazi
Dkt. Yonazi ameeleza kuwa mipango na mikakati iliyojumuishwa katika Mpango wa Lishe wa muda mrefu imezingatia maeneo ya msingi yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa masuala ya lishe nchini na pia kuonyesha umuhimu wa lishe kama nguzo ya msingi itakayosaidia kufikiwa kwa malengo ya nchi kupitia DIRA 2050
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dkt. Germana Leyna, ameeleza kuwa mchakato wa kuandaa mpango huo unaendelea, huku akibainisha baadhi ya changamoto zinazojitokeza, ikiwemo mwitikio mdogo wa wananchi katika kutoa maoni.
Dkt. Leyna alisema TFNC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kuwepo kwa mpango huu na kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ili kupokea maoni. Aidha, Alisisitiza kuwa maoni ya wananchi ni muhimu katika kuhakikisha mpango huo unaakisi mahitaji na vipaumbele vya lishe vya Watanzania.
Mpango wa Taifa wa Lishe wa Muda Mrefu unalenga kuweka mwelekeo wa kitaifa wa kuboresha hali ya lishe nchini kwa kipindi cha miaka 25 ijayo, kupitia ushirikiano wa sekta mbalimbali na mikakati itakayosaidia kuimarisha lishe na ustawi wa Watanzania.
