Kitabu cha Mwongozo wa Chakula na Ulaji Tanzania Bara kimezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Batilda Buriani, tarehe 16 Oktoba 2026, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani
Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), pamoja na wataalamu na wadau mbalimbali kutoka sekta za afya, kilimo, elimu na utafiti.
Wadau wengine walioshiriki ni pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI), Wizara ya Elimu, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na taasisi nyingine za serikali na wadau wa lishe na afya ya jamii ambapo ushirikiano huo unalenga kuhakikisha mwongozo unazingatia ushahidi wa kitaalamu na hali halisi ya maisha ya Watanzania.
Mwongozo huo unasisitiza umuhimu wa kula mlo kamili wenye vyakula mchanganyiko kutoka katika makundi mbalimbali ya chakula yakiwemo nafaka, mizizi na ndizi za kupika, mbogamboga, matunda, jamii ya kunde, karanga na mbegu, vyakula vyenye asili ya wanyama, pamoja na maziwa na bidhaa zake.
Aidha, mwongozo huo unatoa elimu kuhusu usafi na usalama wa chakula, kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na mafuta yasiyofaa, pamoja na umuhimu wa kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Mwongozo unatarajiwa kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu chakula na ulaji, kwa kuzingatia mahitaji ya lishe ya watoto, wajawazito, wanawake wanaonyonyesha na makundi mengine ya jamii, kwasasa kitabu hicho kinapatikana katika tovuti za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)
