SERIKALI YAZINDUA RIPOTI YA HALI YA LISHE UPANDE WA VITAMINI NA MADINI NCHINI (2022 TDHS –MICRONUTRIENTS)
27 Nov, 2026
SERIKALI YAZINDUA RIPOTI YA HALI YA LISHE UPANDE WA VITAMINI NA MADINI NCHINI (2022 TDHS –MICRONUTRIENTS)

DAR ES SALAAM: Serikali imezindua rasmi Ripoti ya Hali ya lishe Tanzania ya mwaka 2022 (TDHS 2022), inayotoa tathmini ya changamoto ya upungufu wa vitamini na madini miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano na wanawake walio katika umri wa uzazi ikiwemo wanawake wajawazito.

Ripoti hiyo imezinduliwa leo, Novemba 27, 2026, na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bruno Sunguya, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Sunguya ameipongeza Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao uliofanikisha maandalizi na kukamilika kwa ripoti hiyo. 

"Matokeo ya ripoti hii ni nyenzo muhimu kwa Serikali katika kupanga na kufanya maamuzi yatakayosaidia kukabiliana na changamoto za upungufu wa vitamini na madini nchini miongoni mwa watoto na wanawake" Amesema Prof. Sunguya

Akielezea baadhi ya matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dkt. Germana Leyna, amesema kuwa upungufu wa damu bado ni changamoto kubwa nchini. Amebainisha kuwa utafiti umeonesha uwepo wa visababishi vingine visivyohusiana moja kwa moja na lishe vinavyochangia Kwa kiasi kikubwa upungufu wa damu kwa wajawazito na watoto.

Aidha Dkt. Leyna, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa hatua mbalimbali inazozichua na kufanikisha kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la upungufu wa vitamini A kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Dkt. Leyna amesema kuwa kiwango cha upungufu wa vitamini A kwa kundi hilo kimepungua kutoka asilimia 33 mwaka 2010 hadi asilimia 5, mafanikio yanayochangiwa na juhudi mbalimbali za Serikali, ikiwemo utoaji wa nyongeza ya vitamini A kwa watoto katika vipindi muhimu vya ukuaji.

Ripoti ya Hali ya lishe Tanzania inayotoa tathmini ya changamoto ya upungufu wa vitamini na madini miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano na wanawake walio katika umri wa uzazi   (TDHS 2022), imeandaliwa na TFNC, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na taasisi za kitaifa na kimataifa, zikiwemo Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID),  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Gates Foundation, Nutrition International, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wengine wengi.