03 Sep, 2026
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imeanza kufanya tathmini ya awali (baseline assessment) ya Mradi wa Lishe Yangu, unaolenga kuboresha huduma za lishe kwa wanawake wajawazito na watoto mkoani Dodoma.
Tathmini hiyo ilianza tarehe 31 Agosti 2026 katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa mama na mtoto vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Katika hatua ya awali, timu ya TFNC imekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, katika ofisi yake iliyopo Jengo la Mkapa jijini Dodoma.
Dkt. Kazungu amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za lishe, hususan kwa wanawake wajawazito na watoto, akieleza kuwa lishe bora ni msingi muhimu wa afya na maendeleo ya jamii.
Mradi wa Lishe Yangu unatekelezwa katika mikoa mitano ambayo ni Dodoma, Mbeya, Songwe, Njombe na Tabora. Tathmini hiyo itasaidia TFNC kupata taarifa za msingi kuhusu hali ya utoaji wa huduma za lishe, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuboresha huduma hizo.
Aidha, timu ya TFNC itatoa mafunzo kwa Timu za Afya na Lishe katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri, kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utoaji wa huduma bora za lishe na kuimarisha utekelezaji wa afua za lishe katika vituo vya afya na jamii.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Rutachunzigwa, amesema tathmini hiyo itasaidia kubaini hali halisi ya huduma za lishe katika vituo vya afya na kuwezesha kubuni mikakati inayolenga kuboresha huduma hizo na kuongeza tija kwa wananchi, hususan wanawake wajawazito na watoto.
