Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), kwa kushirikiana na Shirika la Nutrition International (NI), inatarajia kushiriki katika Mkutano wa 13 wa Tanzania Health Summit 2026 na kuendesha kongamano maalumu kuhusu ajenda ya lishe na mustakabali wa lishe nchini.
Akizungumza leo tarehe 29/9/2026 mara baada ya mkutano wa THS, wadau na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango ya Lishe (TFNC), Bi. Deborah Charwe, amesema TFNC itaendesha kongamano maalumu siku ya Jumanne, Oktoba 6, 2026, litakalojikita katika kujadili masuala ya kimkakati yatakayojumuishwa katika Mpango wa Taifa wa Lishe wa Muda Mrefu ambao unaandaliwa na TFNC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
Amesema kongamano hilo litawakutanisha wataalamu na wadau wa lishe kutoka maeneo mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha lishe kama ajenda ya msingi katika maendeleo ya taifa, ikiwemo kuimarisha mifumo ya chakula ili kujenga nguvu kazi yenye afya na tija itakayochangia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha kongamano hili ni fursa kwa wadau wa afya na lishe katika kujadili namna ambavyo kama nchi tunaweza kuibeba lishe kama agenda ya msingi katika kufikia malengo ya kitaifa kama yalivyoainishwa kwenye DIRA 2050. Aidha wadau watajadili kwakina namna ya kuimarisha mifumo ya chakula ambayo ni endelevu na humilivu na itakayosaidia upatikanaji wa lishe bora katika jamiii pamoja na njia mbalimbali zitakazoweza kukuza uwekezaji wa ndani na kutumia tafiti za kisayansi katika kutekeleza masuala ya lishe nchini
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Mradi wa Urutubishaji wa Vyakula (Food Fortification) kutoka Shirika la Nutrition International (NI), Bi. Mariam Nakuwa, amesema NI itashirikiana na TFNC katika kuendesha kongamano hilo ili kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali kutoa maoni na mapendekezo yatakayozingatiwa katika mchakato wa maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Lishe wa Muda Mrefu.
Mkutano huo wa Tanzania Health Summit (THS), wadau na waandishi wa habari umefunguliwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea na umetoa nafasi kwa wadau kujadili masuala mbalimbali kuelekea mkutano huo muhimu.
