07 Oct, 2025
Tanzania imekuwa nchi ya 26 Barani Afrika kujiunga na juhudi za kikanda za kukabiliana na Utapiamlo wa watoto kupitia sera na uwekezaji unaotegemea takimu mara baada ya kuzindua rasmi Utafiti wa COHA “almaarufu kama Utafiti wa Gharama za Utapiamlo, Septemba 3, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa Kilele cha Mkutano Mkuu wa Wadau wa Lishe nchini.
Tafiti zilizopita za COHA katika nchi 25 za Afrika zimebaini upotevu wa Pato la Taifa wa kila mwaka unaofikia kati ya asilimia 1.9 hadi 16.5 kutokana na athari za muda mrefu za utapiamlo.
Utafiti wa COHA umeongozwa na Serikali ya Tanzania na umehusisha Tanzania Bara na Zanzibar na umetekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Chakula Duniani (WFP) Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF), Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika – Mpango wa NEPAD (AUDA-NEPAD), na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Amerika ya Kusini na Karibiani (ECLAC)
