Tanzania kuanza kuzalisha vyakula vya nyongeza kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5.

News Image

Imewekwa: 28th Aug, 2020

Na TFNC - Morogoro: Tanzania iko mbioni kuachana na kuagiza vyakula vya nyogeza kwa Watoto kutoka nje ya nchi na matokeo yake vitaanza kuzalishwa hapa hapa nchini, mara baada ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na MUHAS, SUA na TBS kuja na mradi wa kutengeneza vyakula vya nyongeza kwa ajili ya Watoto chini ya umri wa miaka mitano, ili kuhakikisha wanapata chakula kilichoboreshwa na kinachokidhi mahitaji yao.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi huo Mkoani Morogoro Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Edward Mbanga kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hadi sasa hakuna uzalishaji wa kibiashara wa vyakula vya nyongeza hapa nchini na badala yake vimekuwa vikiagizwa kwa wazalishaji mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Mbanga alisema Mradi huo ambao unafadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) utahusisha vyakula vya nyongeza vinavyopatikana nchini, ambavyo vimetajwa pia vitasaidia kuboresha matibabu ya Utampiamlo wa kadiri na vitatoa ajira kwa Watanzania watakaozalisha vyakula hivyo.

“Mradi huuu utakuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani Utengenezaji wa vyakula vya nyongeza kwa ajili ya Watoto chini ya miaka mitano utasiadia kuzuia na kutibu utapiamlo wa kadiri nchini, na ni wazi vyakula vitakavyohusika ni vile ambavyo vinapatikana nchini”. Alisema Mbanga

Awali akiwasilisha taarifa za namna mradi huo utakavyotekelezwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dk. Germana Leyna alisema mradi huo utasaidia kuongeza upatikanaji rahisi wa chakula kilichotengenezwa ndani ya nchi kikiwa salama kuweza kuwapatia Watoto lishe bora.

Dk. Leyna alisema pia vyakula hivyo vitaweza kupatikana kwa gharama nafuu na wameamua kufanya hivyo ili kuwezesha kila Mtanzania kuweza kumudu gharama zake na kuweza kumudu kukipata pindi atakapokihitaji.