Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya chumvi yenye madini joto

Imewekwa: 3rd Aug, 2020
Katika kuhakikisha Tanzania inapanda zaidi katika viwango vya kitaifa vya matumizi ya chumvi yenye madini joto, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imeendeleaa kutoa elimu kwa umma, na kuhamasisha wadau mbalimbali kuendelela kusisitiza matumizi ya chumvi yenye madini joto toshelevu ili kuepuka matatizo yanayotokana na upungufu wa madini hayo.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema hivisasa wameanza kutoa elimu na kusisitiza matumizi ya chumvi yenye madini joto, hususani kwa kushirikisha vyombo vya habari mbalimbali nchini kutokana na kuwa na uwezo wa kuwafikia watu wengi zaidi.
Dkt. Germana amesema Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imeanza mchakato wa kutoa elimu kwa kutoa Semina kwa waandishi wa habari 30 kutoka vyombo mbalimbali nchini, ikilenga kudhibiti tatizo la upungufu wa madini joto hapa nchini.
“Semina hii itatoa fursa kwa waandishi kupata uelewa kuhusu masuala ya udhibiti wa tatizo la Upungufu wa madini joto mwilini na pia kuendeleza elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia chumvi yenye madini joto ili kuepuka madhara yatokanayo na tatizo hili” amesema Dkt. Germana.
Kwa mujibu wa Utafiti wa hali ya Demografia na Afya (TDHS), zinaonyesha kuwa kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto toshelevu zimeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2010 hadi asilimia 61 mwaka 2015.