Taasisi kuendelea kushirikiana na wadau kukuza afua za uongezwaji virutubishi kwenye vyakula

News Image

Imewekwa: 24th Feb, 2024

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutambua njia bora za kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika afua za uongezwaji wa viritubishi kwenye vyakula ili kupambana na changamoto za utapiamlo wa kupungukiwa Vitamini na Madini.

Mpaka sasa inakadiriwa asilimia 70 hadi 90 ya Vyakula vinavyosindikwa hapa nchini katika viwanda vikubwa vinaongezwa virutubishi hususani unga wa ngano, mafuta ya kula na chumvi na changamoto imebakia kwenye unga wa mahindi kwani ni asilimia 7 pekee ya unga unaozalishwa ndiyo umerutubishwa.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 22 Februari 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, wakati wa ufunguzi wa kikao cha 37 cha Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula Nchini, kilichofanyika Mkoani Morogoro.

Dkt. Germana amesema Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye vyakula likiongozwa na Wizara ya Viwanda na Biashara limekutana kujadili miakati ya kuongeza ufahamu juu ya afua hiyo ya pamoja na namna ya kuongeza uzalishaji unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kula na chumvi iliyorutubishwa nchini ili kupambana na changamoto za Utapiamlo wa kupungiwa Vitamini na Madini.

Aidha Dkt. Germana amesema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha asilimia kubwa ya unga wa mahindi unaongezwa virutubishi vya vitamini na madini na tayari mpaka sasa zaidi ya vifaa 1026 vya kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi vimeshafungwa na Shirika la SANKU kwenye mikoa 26 nchini.

Kwa upande wake Afisa Biashara Mwandamizi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara anayesimamia Lishe Bwa Festo Kapela, amesema Wizara imeendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali katika suala la uongezaji wa virutubishi kwenye chakula ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa vyakula vinaoongezwa virutubishi vya madini na vitamini nchini.

Kapela amesema kwa sasa tayari Wizara imeandaa rasimu ya kanuni za uongezaji wa virutubishi na inakuja kujibu changamoto zote ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye suala la vyakula vilivyoongezwa virutubishi.