​Serikali Yasisitiza Ushirikiano na Sekta Binafsi Kuimarisha Lishe Nchini.

News Image

Imewekwa: 9th Sep, 2025

Na, Mwandishi wetu Dodoma.

Serikali imesisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi na wadau wengine katika utekelezaji wa afua za lishe ili kukabiliana na changamoto ya utapiamlo nchini.

Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. Paul Sangawe amesema kuwa kila mdau anapaswa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe unakuwa na ufanisi unaotarajiwa.

“Kila mdau na sekta binafsi kwenye eneo hili la lishe ni muhimu ashirikishwe, ili kupata michango ya mawazo, maoni na ushauri katika kuimarisha utekelezaji wa mpango huu,” alisema Bw. Sangawe katika kikao cha wakurugenzi wa lishe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika kikao hicho, wajumbe walipokea na kujadili ripoti mbalimbali ikiwemo: Ripoti ya mapitio ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe, Utafiti wa Gharama za Utapiamlo (Cost of Hunger - COHA), Maadhimio ya Mkutano wa 10 wa wadau wa lishe nchini, pamoja na kujadili taarifa ya Maandalizi ya Mkutano wa 11 wa Wadau wa Lishe unaoarajiwa kuifanyika mwaka huu.