Serikali kuwekeza katika lishe ili kukabiliana na utapiamlo

News Image

Imewekwa: 9th Jun, 2022

Serikali imeahidi kufanya Uwekezaji Kitaifa katika masuala ya lishe nchini kama sehemu ya mapambano dhidi ya Utapiamlo kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kushiriki kikamilifu katika shughuhuli za uzalishaji.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu wakati wa kikao kazi kilichohusisha Watendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) pamoja na wadau wa maendeleo kuhusu Masuala ya Lishe nchini katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Juni 08, 2022 Bungeni Jijini Dodoma.

Mhe. Simbachawene alisema kama Taifa ni muhimu kuweka jitihada za pamoja katika mapambano hayo kwani matatizo ya kilishe yamekuwa na madhara makubwa kwa watanzania hivyo kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji kwa ufanisi.

“Uwekezaji kama Taifa katika lishe ni muhimu sana ipo mikoa mingi inazalisha chakula kwa kiwango kikubwa kama Iringa na Mbeya lakini kuna shida kubwa ya utapiamlo hasa kwa watoto na changamoto hiyo inasababisha hasara kwa jamii na Serikali,” alisema Mhe. Simbachawene.

Pia aliongeza kwamba ipo haja ya elimu ya lishe kufundishwa katika shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ili kuwandaa vijana kuwa mabalozi wazuri wa lishe katika maeneo yao au hata watakapofikia hatua ya kujitegemea.

“Unapokosa lishe nzuri unapata matatizo ya afya, kina mama wajawazito kukosa afya bora na watoto kuwa na udumavu wa akili na mwili na Serikali itapata hasara kwa sababu ya kuwa na watu wasiyo na afya bora kutokana na maradhi kwa kukosa lishe bora,” aliongeza.

Aidha alisisitiza ushirikishwaji wa viongozi wa Serikali za mitaa,vijiji na vitongoji, wakuu wa wilaya na Mikoa kwa kuwapatia elimu ya lishe itakayowasaidia kuwafikia wananchi katika maneo yao ili kuwa na matokeo chanya na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Viongozi hawa wakipatiwa elimu ya lishe bora nini mtu ale, vyakula gani vya muhimu maana watu wanaweza kufikiri kula chakula bora lazima uwe na uwezo la hasha! chakula kwa uwezo wowote unaweza kupangilia kikawa na tija katika mwili wako je, uelewa huu upo mpaka ngazi za chini ? Je, nani afuatilie kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora lazima tutumie ngazi hizi za utawala kujenga Taifa letu,” alisisitiza Mhe. Simbachawene.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Germana Leyna (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe nchini katika kikao hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CHakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna alisema wataendelea kushirikiana na Serikali, kushauri, kuongoza na kuhamasisha lishe bora ili kuhakikisha malengo ya Nchi yanafikiwa ambayo ni kufikia maendeleo endelevu.

“Hatuwezi kufikia malengo kama hakuna ujumuishwaji wa lishe katika sera, mipango, kuimarisha uratibu na kuhamasisha masuala ya lishe na miradi mbalimbali ya lishe kuifikia jamii kwa wingi zaidi,” alibainisha Mkurugenzi huyo.