Naibu Waziri azindua mwongozo wa utekelezaji wa Siku ya Afya na Lishe Kitaifa

News Image

Imewekwa: 31st Oct, 2022

Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel amezindua Mwongozo wa Utekelezaji wa Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji pamoja na makala maalumu ya kuhamasisha wadau na viongozi mbalimbali kusimamia na kutekeleza siku hiyo katika maeneo yao. Dkt. Mollel amezindua Mwongozo huo wakati akimuwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika tarehe 29/10/2022 katika uwanja wa mpira wa miguu Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoa wa Morogoro.

“Niipongeze Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuongoza harakati za kukabiliana na utapiamlo nchini ikiwemo uandaaji wa mwongozo huu unaohusu utekelezaji wa afua za lishe vijijini ambao leo tunauzindua tukiwa katika kijiji cha Mikese, na wala hatuzindui mwongozo unaohusu masuala ya kijiji tukiwa mjini, hongereni sana” amesema Dkt. Mollel.

Aidha Dkt. Mollel amewataka wadau wa lishe kuongeza jitihada zaidi za kukabiliana na utapiamlo nchini kwa sababu sasa Tanzania inakabiliwa na aina mpya ya utapiamlo wa lishe iliyozidi ambayo inachangia katika kuongeza kasi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwemo kisukari, magonjwa ya moyo, figo na baadhi ya saratani.

Awali akitoa salamu za Wizara ya Afya, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dkt. Beatrice Mutayoba amesema kuwa Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji ni muhimu katika kuwasogezea karibu wananchi huduma za afya na lishe na hivyo kuchochea mabadiliko ya tabia kwa wananchi katika kutumia huduma za afya na lishe.

“Mheshimiwa Mgeni Rasmi, uzoefu unaonesha kuwa kwa maeneo ambayo wamekuwa wakitekeleza siku ya afya na lishe ya kijiji kumekuwa na ongezeko la matumizi ya huduma za afya kwa wananchi, kwa mfano mkoani Dodoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba akinamama wanaohudhuria kliniki wameongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 2014 hadi asilimia 52 mwaka 2018” Amesema Dkt. Beatrice.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Dkt. Esther Nkuba wakati akitoa salamu za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kwa mara ya tatu tangu yalipoanza kuadhimishwa mwaka 2020. Dkt. Nkuba amesema maadhimisho hayo yanasaidia kuwakutanisha wadau na wananchi na hivyo wananchi kupata huduma mbalimbali za afya na lishe, ikiwemo kupimwa hali za lishe, kupata elimu na ushauri wa masuala ya chakula na lishe.

Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu inayosema “Lishe Bora ni Msingi wa Maendeleo Endelevu: Sote Tuwajibike”