Mtaalamu aelezea mbinu za kujikinga na ugonjwa wa kiharusi

News Image

Imewekwa: 29th Oct, 2019

Wakati Shirika la Afya Dunia (WHO) likionesha kuwa katika kila watu wanne, mmoja yupo kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi, Afisa lishe Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bi. Adelina Munuo amewashauri watanzania kuzingatia ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ikiwemo kuacha kutumia vyakula vyenye mafuta kwa wingi na kupunguza matumizi ya chumviiliyopitiliza, ili kuweza kuepukana na ugonjwa huo.

Aidha Munuo amezitaja mbinu nyingine za kujikinga na ugonjwa huokuwa ni kufanya mazoezi angalau kwa muda wa nusu saa kila siku, kuzuia na kutibu shinikizo la damu, kudhibiti kisukari, kupunguza au kuacha kunywa pombe kupita kiasi pamoja na kuepuka matumizi ya tumbaku na sigara.

Munuo amesema Kiharusi ni Ugonjwa unaotokanana mishipa inayosambaza damu kwenye ubongo kupatwa na misukosuko kiasi cha kushindwa kupeleka damu kwenye ubongo na hivyo kuathiri ufanyaji kazi wa ubongo kwa zaidi ya masaa 24.

Akizungumzia Dalili za Ugonjwa wa Kiharusi Bi. Munuo amesema zipo dalili mbalimbali za ugonjwa huo hata hivyo dalili zake huweza kujitokeza kwa kutegemea sehemu ya Ubongo iliyoathiriwa, ikiwa kuanzia, sehemu ya ubongo mkubwa (Celebellum), sehemu ya kati (Cerebral Cortex) na hata endapo mgonjwa atakuwa ameathirika sehemu ya ubongo kwenye shingo kuelekea kwenye uti wa mgongo.