Mkurugenzi Mtendaji TFNC akutana na Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha New York

News Image

Imewekwa: 30th Jul, 2023

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna akiwa na Menejimenti ya Taasisi, amekutana na kufanya mazungumzo na mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha New York kilichopo nchini Marekani Prof. Amr Soliman na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo la kuanzisha ushirikiano na Chuo hicho, utakaosaidia kubadilisha uzoefu na kusimamia wanafunzi watakaokuwa wanakuja nchini kusoma kwa vitendo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana amesema kuwa ushirikiano watakaouanzisha utasaidia Taasisi kupanua wigo wa kufanya tafiti na kutengeneza chakula maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa Saratani wanaopata tiba kwa njia ya Mionzi.

“Saratani ni moja ya magonjwa yanayoongezeka kwa kasi hapa nchini. Serikali yetu chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani umechukua hatua kubwa katika kukabiliana na ugojwa huu. Hivyo tunaamini TFNC kupitia ushirikiano huu ambao tunaenda kuuanzisha tutaongeza mchango wetu katika kukabiliana na ugonjwa wa saratani, kwa kufanya tafiti zitakazotoa majibu chanya lakini pia kwa kutengeneza chakula maalumu kwa wagonjwa wanaotibiwa kwa mionzi na kisha kupata changamoto katika ulaji wao” Amesema Dkt. Germana.

Kwa upande wake Prof Soliman wa Chuo Kikuu cha New York amesema ushirikiano watakaoingia na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, utawasaidia katika kubadilishana uzoefu walionao katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali hususani zile ambazo zimelenga kuangalia uhusiano uliopo kati ya lishe na kuongezeka kwa magonjwa ya saratani, hususani saratani ya koo na saratani ya utumbo mpana.