27 Oct, 2025
Mikoa ya Simiyu na Manyara imeongezwa katika mikoa ambayo itatekeleza utafiti wa majaribio ya mfumo wa ufuatiliaji taarifa za matumizi ya chumvi yenye madini joto (FORTMAS) katika ngazi ya jamii.
Awali Utafiti huo ulikuwa umeanza kufanyika katika mikoa mitatu ya Singida, Mtwara na Dar es Salaam ukitekelezwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania wakishirikiana na Shirika la Iodine Global Network (IGN) na sasa mikoa hiyo miwili hiyo inaongezeka ili kuongeza eneo la utafiti huo ambao unalenga kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa taarifa za matumizi ya chumvi yenye madini joto ngazi ya Kaya kwa wakati na urahisi zaidi.
Timu ya Watafiti bobezi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Iodine Global Network (IGN), pamoja na Shirika la Nutrition International (NI) wametembelea mkoa wa Simiyu na tayari wameanza kutoa mafunzo elekezi ya namna ya kufanya utafiti huo kwa Waganga wakuu, Maafisa Lishe, Waratibu wa Mama na Mtoto, Wauguzi, Wataalamu wa Maabara na Wataalamu wa taarifa za afya na lishe.
Pamoja na mafunzo hayo, wataalamu hao wamepatiwa vifaa mbalimbali vya kukusanya na kuhifadhi sampuli za chumvi na mkojo kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kimaabara kutambua viwango vya madini joto katika sampuli hizo.
Matokeo ya utafiti wa FORTIMAS yatasaidia kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa taarifa chumvi yenye madini joto ngazi ya Kaya kwa wakati na urahisi Zaidi na kupata takwimu muhimu kwa ajili ya kuona mwenendo wa tatizo la Upungufu wa madini joto nchini.
