Mhe.Rais Samia apata Tuzo ya Lishe

News Image

Imewekwa: 25th Oct, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo ya heshima kwa kuwa kinara katika masuala yanayohusu Lishe wakati wa Kilele cha Siku ya Lishe Kitaifa.

Tuzo hiyo ya heshima imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Oktoba 23 wakati wa kuhitimisha kilele cha maadhimisho ya siku ya Lishe ambayo kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika mkoani humo katika viwanja vya Nanenane Ipuli.

Akikabidhi tuzo hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, kwa ajili ya kuiwasilisha tuzo hiyo kwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuendeleza huduma za lishe nchini. Mkuu wa mkoa wa Tabora Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema kuwa Rais amekuwa kinara katika masuala ya lishe kwa kusaini mikataba na wakuu wa mikoa yote nchini ili waweze kusimamia kwa ukaribu shughuli za lishe katika mikoa yao.

“Tumeona hatuna lolote la kumpa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa makubwa aliyoyafanya katika kipindi kifupi lakini kubwa zaidi ni katika hili la lishe ambalo yeye mwenyewe ndio amekuwa muasisi, na ndiye kinara, tunampa tuzo ya heshima, ambayo tunasema mkoa wa Tabora tunampongeza sana kwa kuleta maendeleo makubwa na kuongeza uwajibikaji lakini kwa kuwa kinara wa masuala ya lishe hapa nchini” amesema Mhe. Balozi Buriani.

Itakumbukwa Mwezi Juni, 2021 Rais Samia akiongea na wanahabari nchini kwa lengo la kutathmini hali ya utendaji kazi wa Serikali yake ndani ya Siku 100 alitoa ahadi ya kuendelea kulipa kipaumbele masuala ya lishe nchini, ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha nchi inaondokana na tatizo la utapiamlo, na wananchi wake wanakuwa na afya na lishe bora.

“Kwa sasa nitafanya kazi hiyo nikiwa kwenye kiti hiki cha Urais ambapo najua wakuu wa Mikoa watakwenda kujituma zaidi ili kuondosha tatizo hili, kwani tatizo kubwa tumegundua ni elimu kwa wananchi wetu, lakini wakielimishwa vizuri, wanaelewa” alisema Rais Samia.

Jitihada za Mhe. Rais Samia katika kuendeleza huduma za Lishe zilianza tangu alipokuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2018 alitoa maagizo kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuingia mikataba na wakuu wa mikoa na kisha wakuu wa mikoa kuingia mikataba hiyo na wakuu wa wilaya ili kuboresha shughuli za lishe nchini. OR-TAMISEMI walitekeleza agizo hilo mwezi Disemba, 2018 na kuweka viashiria 11, kama Vigezo vya kutathmini hali ya Lishe nchini.