MAJALIWA: LISHE BORA NI MUHIMU KWA UKUAJI WA UCHUMI

News Image

Imewekwa: 19th Nov, 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 18, 2021) katika Mkutano wa Saba wa Wadau wa Lishe unaofanyika kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort Jijini Tanga. Amesema lishe bora ndio msingi wa makuzi ya kimwili na kiakili kwa watoto na husaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuwa chanzo cha ubunifu katika kazi.

“Maendeleo ya Taifa pamoja na mambo mengine, yanahitaji uwepo wa watu (nguvu kazi) wenye afya njema na lishe bora ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii na tija. Rasilimali watu imara ndio msingi wa kuzalisha kwa tija na kupunguza umaskini. Tutaendelea kuchukua hatua stahiki za Kukabilina na aina zote za utapiamlo”. Alisema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema madhara yanayotokana na udumavu hayana tiba, ni ya kudumu kwa kipindi chote cha uhai wa mtoto aliyeathirika, hivyo ametoa wito kwa Watanzania wote wafuate maelekezo ya wataalam wa afya na kwa pamoja washirikiane kupambana na changamoto hiyo ya udumavu.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhusu lishe ikiwemo kuwa na mipango endelevu ya maendeleo ambayo inazingatia lishe kama moja ya vipaumbele. Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 vimeweka bayana kuwa suala la lishe ni moja ya vipaumbele vyake mahsusi.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI iendelee kusimamia Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatolewa kwa wakati na kutumika katika malengo kusudiwa.