LISHE BORA NI MUHIMU KWA WANAFUNZI- DR. MTAHABWA
Imewekwa: 15th Nov, 2024
Lishe Bora ni muhimu kwa wanafunzi ili kuwawezesha kuwa na afya bora kimwili na kiakili hivyo kuweza kushiriki vema katika masomo.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mtahabwa, Oktoba 28, 2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa lishe shuleni chenye lengo la kujadili na kuandaa mpango kazi utakaowezesha utekelezaji fanisi wa afua za lishe katika shule.
Dkt. Mtahabwa amesisitiza kuwa Suala la lishe shuleni ni muhimu na linahitaji kujadiliwa kwa kina na wadau wote ili kuhakikisha kila mtoto anapata lishe Bora akiwa shule.
"Ili wanafunzi waweze kujifunza vizuri wanahitaji mazingira mazuri pamoja na kuwa na afya bora ya kimwili na kiakili" alisema Dkt. Mtahabwa
Kikao kazi hicho kimehusisha wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Elimu, Ofisi ya Rais Tamisemi, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Wizara ya Fedha, Wizara ya kilimo, Wizara ya Afya, Wizara ya maji, Wizara ya Maendeleo ya jamii, Pamoja Tuwalishe na wadau wengine wa lishe nchini.
Source-Wizara ya ELimu, Sayansi na Teknolojia