05 May, 2026
Mei 4, 2026, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, Wizara ya Elimu Zanzibar pamoja na Wataalamu kutoka Shirika la Iodine Global Network (IGN), imefanya kikao kazi muhimu cha maandalizi ya kuanza rasmi kwa utafiti wa mfumo wa ufuatiliaji wa chumvi yenye madini joto (FORTIMAS) katika ngazi ya jamii.
Lengo ni kuanzisha mfumo rahisi na endelevu wa kukusanya takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kuona mwenendo wa tatizo la upungufu wa madini joto visiwani humo na kuchukua hatua za haraka kulinda afya ya jamii.
Wataalamu wa Lishe kutoka Wizara ya Afya Zanzibar na Wizara ya Elimu Zanzibar, Mei 5, 2026, wametembelea Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza uzoefu wa uchambuzi wa sampuli mbalimbali zinazohusiana na vyakula.
Maabara ya TFNC ni Maabara Rejea inayotambulika na kuaminika kimataifa na mashirika kama WHO, CDC, ECSA-HS, na IGAD, ikiwa ni maabara pekee ya aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati, na Kusini.
Ziara hii ni sehemu ya maandalizi ya utafiti wa mfumo wa ufuatiliaji wa chumvi yenye madini joto (FORTIMAS) visiwani Zanzibar, ili kuhakikisha takwimu zitakazopatikana zina vigezo vya kimataifa kwa ajili ya afya ya wananchi.
