17 Mar, 2026
Kamati ya Taifa ya Wataalam ya Usimamizi na Ushauri wa Masuala ya Lishe imekutana tarehe 16 Machi 2026 katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma, kujadili na kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za lishe nchini ikiwemo Mpango Jumuishi wa kitaifa wa masuala ya lishe pamoja na mikakati mingine ya kuboresha hali ya lishe nchini.
Kikao hicho kimejadili taarifa ya maendeleo ya Mpango Jumuishi wa kitaifa wa masuala ya lishe (NMNAP), maandalizi ya Kongamano la Wadau wa Lishe nchini, pamoja na hatua za kuimarisha ufuatiliaji wa viashiria vya lishe kupitia mradi wa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa viashiria vya lishe nchini Tanzania
Lengo la kikao hicho ni kuendelea kuimarisha uratibu na usimamizi wa juhudi za kuboresha lishe kwa maendeleo ya afya na ustawi wa wananchi.
Kikao kazi hicho kimeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Bw. Paul Sangawe na kushirikisha wataalamu mbalimbali kutoka Wizara, Taasisi, Mashirika na Wadau wa Maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amewasilisha wasilisho la utambulisho wa Mradi wa Kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji wa Viashiria vya Lishe Tanzania (Micronutrient Biomarker Surveillance System in Tanzani -MNBi-URT) mbele ya kamati ya taifa ya Wataalam ya Usimamizi na Ushauri wa Masuala ya Lishe.
