GAIN kuendelea kushirikiana na Serikali kuongeza virutubishi kwenye chakula

News Image

Imewekwa: 24th Jul, 2023

Shirika la Global Alliance For Improved Nutrition (GAIN) limesisitiza litaendelea kushirikiana na Serikali hususani kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, kuendelea kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubishi ikiwemo unga wa Mahindi, Ngano, Mafuta ya Kupikia pamoja na Chumvi.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa programu ya urutubishaji kutoka shirika la GAIN Dkt. Archard Ngemela wakati akizungumza na Maafisa Utafiti wa Taasisi ya chakula na Lishe Tanzania, wakati wa Semina ya majadiliano kuhusu umuhimu wa urutubishaji wa vyakula kwa ngazi ya Viwanda iliyofanyika hivi karibuni.
Dkt.Ngemela amesema shirika la GAIN limejikita zaidi kuhakikisha linasaidia serikali kwenye upatikanaji wa Virutubishi, upatikanaji wa mashine za kuchanganya virutubishi hivyo kwenye unga pamoja na kuwajengea uwezi watendaji wa ngazi za Mikoa na Halmashauri katika usimamizi wa ubora wa urutubishaji.
“Kwa sasa GAIN tumesaidia Serikali kununua mashine 50 ambazo zimetengezwa hapa hapa nchini na SIDO kwa gharama ya Milioni 60, na tutazigawa kwa vyama vya wazalishaji mahindi katika mikoa ya Kagera, Mara, Iringa, Kilimanjaro na Manyara ikiwa ni jitihada za kuisaidia Serikali kufikia malengo ya kununua mashine 300 ili kuboresha huduma ya urutubishaji vyakula nchini.”alisema Dkt.Ngemela
Aidha Dkt.Ngemela amesema kwa upande wa kuwajengea uwezo wataalamu, amesema wameendelea kushirikiana na Serikali kwani hadi sasa tayari wamefanikiwa kuwajengea uwezo wataalamu 120 wakiwemo maafisa lishe, Wataalamu wa maabara na maafisa ya Lishe ambao ndiyo wanasimamia ubora wa vyakula vilivyorutubishwa.
“Tayari tumewafikia Maafisa lishe, Maafisa afya na wataalamu wa Maabara katika mikoa ya Kilimanjaro, Mara, Kagera,na Iringa na kuwajengea uwezo kuhusu namna ya kufanya uchambuzi wa kimaabara ili kubaini viwango vya madini na vitamin kwenye vyakula vilivyofanyiwa urutubishaji.” Alisema Dkt. Ngemela. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amewapongeza GAIN kwa jitihada wanazochukua katika kufanikisha urutubishaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi, na Serikali kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania wako tayari kushirikiana na Shirika hilo katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kutumia vyakula hivyo ili kusaidia Watanzania kuepukana na matatizo ya upungufu wa madini na Vitamini.