WATAALAMU, WADAU WAJADILI AJENDA YA LISHE KATIKA MKUTANO WA 13 WA TANZANIA HEALTH SUMMIT 2026
08 Oct, 2026
WATAALAMU, WADAU WAJADILI AJENDA YA LISHE KATIKA MKUTANO WA 13 WA TANZANIA HEALTH SUMMIT 2026

Dar es Salaam: Jopo la wataalamu wa lishe na wadau mbalimbali limeendesha mjadala maalumu kuhusu ajenda ya lishe nchini, likijadili namna Tanzania inavyoweza kuimarisha umiliki na uendelevu wa ajenda ya lishe nchini kupitia dhana ya “Nutrition Sovereignty”

Mjadala huo wa kitaalamu ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na shirika la kimataifa la Nutrition International (NI) umefanyika tarehe 6 Oktoba 2026 katika Mkutano wa 13 wa Tanzania Health Summit, Mlimani City, Dar es Salaam ambapo wataalamu na wadau walibadilishana uzoefu na mitazamo kuhusu hatua muhimu za kuimarisha mifumo ya lishe nchini.

Akifungua mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna amesisitiza umuhimu wa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ya kaya na jamii katika utekelezaji wa ajenda ya lishe. Aidha, alieleza umuhimu wa kuimarisha mifumo iliyopo ya Serikali za Mitaa katika utekelezaji, ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za lishe, badala ya kuanzisha mifumo mipya.

Katika mjadala huo, washiriki pia walijadili kuhusu Mpango wa Taifa wa Lishe wa Muda Mrefu kwa miaka 25 ijayo. Katika ajenda hii wadau walipata fursa ya kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine zilizowahi kuandaa mipango ya muda mrefu ya lishe, ikiwemo Ethiopia, na kutathmini uzoefu huo katika muktadha wa Tanzania.

Aidha, washiriki na wadau walioshiriki katika mjadala huo walitoa maoni na mapendekezo kuhusu maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika Mpango wa Taifa wa Lishe wa Muda Mrefu, ambao kwa sasa uko katika hatua ya maandalizi.

Kwa ujumla, mjadala huo umeonesha umuhimu wa kuunganisha sera na mipango ya kitaifa na uhalisia wa maisha ya kaya na jamii, huku ushiriki wa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine ukiwa muhimu katika kujenga Tanzania yenye afya na lishe bora kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.