Wadau wa lishe wahimizwa kuendelea kuisaidia serikali kwenye tafiti za lishe

News Image

Imewekwa: 12th Jun, 2024

Wadau na wafadhili wa shughuli za lishe nchini, wameshauriwa kujitokeza na kuisaidia Serikali rasilimali fedha, na msaada wa kitaalamu katika kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na masuala ya Chakula na lishe zinazolenga kutatua matatizo ya kilishe yaliyopo katika jamii ya watanzania.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 11, 2024 na Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume, wakati akizungumza na Maafisa wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kutoka New York nchini Marekani, na UNICEF Tanzania mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Taasisi hiyo, hususani uongezaji wa madini joto katika chumvi.

Mbali na ziara hiyo wageni hao pia wamefanikiwa kukutana na wadau mbalimbali wa chumvi na kuweza kujadili kwa pamoja namna wanavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohusiana na uongezaji wa madini joto kwenye chumvi inayozalishwa nchini.

“Tunaomba wadau waangalie namna gani wanaweza kuisaidia Serikali kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kuipitia rasilimali fedha na msaada wa kitaalamu utakaoiwezesha Taasisi hiyo kufanya tafiti nyingi iwezekanavvyo, tafiti ambazo zitasaidia utekelezaji wa afua mbalimbali za kilishe hapa nchini.”amesema Dkt. Mfaume.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amesema ujio wa wageni hao kutoka USAID na UNICEF utaenda kuleta tija katika eneo la ushirikiano la utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kilishe nchini, ikiwemo kuimarisha shughuli za usimamizi wa uongezaji wa madini joto kwa chumvi yote inayozalishwa na nchini.

Dkt. Leyna amesema kwa pamoja wamejadili maendeleo ambayo yamepatikana kutokana na program ya uongezaji wa madini joto katika chumvi toka kuanzishwa kwake miaka ya 90, na wanaona kuna maendeleo makubwa katika utekelezaji wa programu, kutokana na kutambua mbinu mbalimbali ambazo zimeweza kuhamaisha kuongezeka kwa uzalishaji wa chumvi iliyoongezwa madini joto kutokana na usimamizi mzuri kuanzia ngazi ya taifa hadi Halmashauri.