TUMETEKELEZA VIZURI MKATABA WA LISHE 2024/25 - PROF. SHEMDOE
25 Jan, 2026
TUMETEKELEZA VIZURI MKATABA WA LISHE 2024/25 - PROF. SHEMDOE
Na OWM- TAMISEMI:   Tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/25 imeonesha mafanikio makubwa, ambapo rangi ya kijani imetawala katika viashiria vingi vya utekelezaji, ikiwa ni ishara ya kufanya vizuri kwa mikoa na halmashauri nchini. Hayo yamesemwa leo Januari 22,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, wakati akifungua mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/25. Prof. Shemdoe amesema Taifa limeendelea kupiga hatua kubwa katika kuboresha hali ya lishe kwa wananchi, hali inayochangia kuimarisha nguvu kazi yenye afya bora na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. “Nawashukuru Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa pamoja na viongozi na watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri kwa kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu na kutekeleza Mkataba wa Lishe,” amesema Prof. Shemdoe. Amewahakikishia kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI itaendelea kushirikiana na kuwapa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa matatizo ya lishe nchini inafikiwa. Amebainisha kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa wosia wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyehimiza kuimarishwa kwa sekta za Elimu, Afya na Uchumi ili kupambana na maadui watatu wa Taifa ambao ni ujinga, maradhi na umasikini. Prof. Shemdoe amesema uwekezaji katika lishe ni mkakati wa kiuchumi wenye tija kubwa, na kwamba Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeipa kipaumbele kujenga jamii yenye afya kwa kuzingatia lishe bora ili kila mwananchi astawi.