Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania yazindua Mkataba wa Huduma kwa Wateja

Imewekwa: 11th May, 2022
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amezindua rasmi Mkataba wa Huduma kwa Wateja wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ambao lengo lake ni kuweka makubaliano kati ya Taasisi na wateja juu ya wigo na viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa ili kukidhi matarajio yao.
Akizindua Mkataba huo katika hafla fupi iliyofanyika katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Prof. Makubi amesema Mkataba huo una manufaa kwa Taasisi za Umma kwa ujumla ikiwemo wananchi kupata huduma kwa wakati na bila upendeleo kwani Taasisi zitalazimika kufuata viwango vilivyowekwa kwenye mkataba huo.
Prof. Makubi amesema kuna baadhi ya Taasisi zimekaa muda mrefu bila kuwa na Mkataba wa Huduma kwa wateja licha ya utekelezaji wa mpango huu kuanza toka mwaka 2001 ambapo Taasisi zilitakiwa kutumia mikataba hii kwa utekelezaji wa majukumu yenye ufanisi na tija zaidi hivyo kutoa muda wa miezi mitatu kuhakikisha Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Hospital za Kanda, Taifa na Mikoa kuhakikisha zinakuwa na Mikataba ya Huduma kwa Wateja.
“Wateja wetu wanaenda Hospital na hawajui vipimo watapatiwa lini, unaenda maabara haujui majibu utayapata lini, matokeo yake inamlazimu mgonjwa kutumia njia zisizo rasmi”. alisema Prof. Makubi
Awali akitoa neno la Ukaribisho Mkurugenzi Mtendaji wa Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema Mkataba huo utawawezesha wateja wa Taasisi hiyo kuzifahahmu huduma zinazotolewa na Taasisi na utaiwezesha Taasisi kuboresha huduma zake kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu na pia kupata maoni au malalamiko kutoka kwa wateja na kuyashughulikia kwa wakati.
“Lengo la Mkataba huu ni kuweka makubaliano kati ya Taasisi na wateja wetu juu ya wigo na viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa ili kukidhi matarajio yao”alisema Dkt. Germana
Kwa upande wake Mwenyekiti Bodi ya usimamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Obey Assery amesema ameipongeza Menejimenti ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kuhakikisha wameandaa mkataba wa huduma kwa wateja kwani utaisaidia kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa kufuata viwango na hivyo kuwezesha Taasisi kutekeleza matakwa ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.
Akitoa salamu kutoka kwa wadau wa lishe nchini Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali PANITA Tumaini Mikindo amesema hatua iliyochukuliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ni muhimu kwani inamuwezesha mteja kufahamu ni huduma gani atazipata kwenye Taasisi hiyo na huduma gani hatozipata hivyo kumuondolea usumbufu wa kutafuta huduma hizo.
Mwaka 2001 Serikali ilianzisha utaratibu wa kutumia mikataba ya utoaji huduma kwa wateja ili kusaidia katika utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na tija zaidi na mwaka 2013 Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilitoa mwongozo katika utekelezaji wa mikataba ya utoaji wa huduma kwa wateja katika Taasisi za umma.
MWISHO.