Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, aridhishwa na Utendaji Kazi wa Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania

Imewekwa: 15th Jun, 2022
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amefanya ziara ya kikazi katika Maabara ya kupima Virubishi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania na kuridhishwa na utendaji kazi wa maaabara hiyo katika kupima sampuli mbalimbali za vyakula, zikiwemo sampuli zinazotumika katika tafiti mbalimbali zinazohusiana na masuala ya Chakula na Lishe.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maabara ya Taasisi hiyo Dkt. Shekalaghe amesema maabara hiyo inapima sampuli kutoka nchi mbalimbali na ina mashine za kisasa ambazo hazipo kwenye nchi za Afrika Mashariki na kati, hivyo kuwashauri wajasiriamali wanaojihusisha na biashara za vyakula, kupelekea bidhaa zao katika maabara hiyo kupima kiwango cha viini lishe vinavyopatikana katika bidhaa zao, ili kuwasaidia kuzalisha bidhaa bora zaidi.
“Maabara hii ina mashine zenye uwezo mkubwa na inapokea sampuli kutoka nchi mbalimbali kwani mashine zilizopo katika maabara hii hazipo katika nchi za Afrika Mashariki na kati, hivyo inatakiwa hii maabara watu wengi waweze kuifahamu na iweze kutumika, hususani kwa wajasirimali wanaojihusisha na biashara ya vyakula, alisema Dkt .Shekalaghe.
Aidha Dkt. Shekalaghe amesema Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imekuwa maabara muhimu katika tafiti mbalimbali za kitaifa katika upande wa masuala ya Chakula na Lishe ambazo zimesaidia kuishauri Serikali namna ya kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na matatizo ya Kilishe yaliyopo nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Usimamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bw. Obey Assery amesema wanaendelea kufanya kazi sambamba na Taasisi hiyo na kuisimamia kuhakikisha inatekelezaji sera, Mikakati, Sheria, Kanuni na taratibu zinatekelezwa kwa ajili ya ustawi wa lishe ya nchi hii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema bado kuna mwamko mdogo kwa wajasirimali kujitokeza kufanya vipimo vya bidhaa zao za vyakula katika maabara hiyo, hivyo kuwashauri kufika kuweza kupatiwa huduma hizo kwani zitawasaidia kuboresha bidhaa zao katika soko la ushindani.
Maabara ya Kupima viini lishe iliyopo chini ya usimamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ilianzishwa toka Mwaka 1980 na imekuwa ikitoa huduma ya kupima sampuli za vyakula na sampuli za kibolojia za binadamu ili kuweza kuangalia hali ya lishe, na imekuwa ikipokea sampuli kutoka nchi mbalimbali ikiwemo nchi za Afrika Mashariki na kati pamoja na nyingine kutoka Ulaya ya Mashariki.