Kampeni ya lishe bora kwa njia ya daladala yazinduliwa rasmi
Imewekwa: 5th Jun, 2024
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), wamezindua rasmi kampeni ya Lishe Bora kwa Njia ya Daladala, ikilenga kuongeza uelewa kwa wanajamii wote juu matumizi sahihi ya chakula ili kuhamasisha ulaji unaofaa kwa kila mmoja na kuweza kupunguza matatizo ya kilishe miongoni mwa Watanzania.
Uzinduzi huo ambao umefanyika katika kituo cha Daladala cha Makumbusho, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Lishe huku Mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Saadi Mtambule, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila.
Akizungumza katika Uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema, kampeni hiyo ni moja ya mbinu ya kuwezesha kutoa elimu ya Mtindo bora wa maisha, ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mwongozo wa Taifa wa Chakula na Ulaji, ulioanzishwa kwa lengo la kuhimiza uzalishaji na ulaji wa vyakula mchanganyiko vinavyokubalika katika jamii.
“Elimu itakayotolewa ndani ya daladala itazingatia ushauri wa kitaalamu kutoka kwenye Mwongozo wa kitaifa wa Chakula na Ulaji wa Tanzania Bara kwa kuzingatia Mapendekezo ya makundi sita ya chakula pamoja na utayarishaji na uhifadhi usalama wa chakula, kushughulisha mwili na kuepuka tabia hatarishi, Amesema Dkt. Germana
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Saadi Mtambule,amesema agenda ya lishe imepewa kipaumbele katika maeneo yote, hivyo wao kama serikali ya mkoa watahakikisha kampeni hii inatekelezwa ipasavyo, ili kuweza kufikisha elimu iliyokusudiwa kwa watu wengi zaidi.
Kampeni ya Lishe bora kwa njia ya daladala itaendeshwa kwa muda wa mwezi mmoja katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam zikihusisha watu wazima na watoto/vijana wa shule za msingi na sekondari kwa utaratibu maalum uliowekwa, Aidha Mkoa wa Mbeya na Unguja kwa Tanzania visiwani nao watanufaika sambamba na kampeni hii.