Chuo kikuu cha TSING HUAN na TFNC zaungana kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu kwa vijana balehe

News Image

Imewekwa: 9th Jun, 2024

Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Tsing Huan cha nchini China, wapo katika utekelezaji wa mradi wa majaribio wa utengenezaji asusa zilizoongezwa madini na Vitamini (Zinki, Magneziamu, Vitamini A n.k) zitakazotumiwa na watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 19 lengo likiwa kusaidia kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu kwa vijana wa rika balehe.

Akizungumza leo Juni 7, 2024 jijini Dar es Salaam, mara baada ya kupokea ugeni wa maafisa kutoka Chuo Kikuu cha Kikuu cha Tsing Huan, waliotembelea Taasisi ya Chakula na Lishe kujionea utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema mradi huo unaenda kutatua changamoto za kilishe ambazo wanapitia vijana balehe.

“Wataalamu wameweza kutengeneza formulation ambayo itatumia maharage ambayo yamerutubishwa na Zinki pamoja na madini chuma, mahindi ya njano kwa ajili ya kutengenezaBiskutit, kwa sasa tupo katika hatua ya awali ya kupeleka mashuleni ili kupata mrejesho” amesema Dkt. Leyna.

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt, Anselm Moshi, amesema mradi uwa majaribio umedumu kwa muda wa mwaka mmoja na matarajio yaliyopo ukikamilika asusa hizo zitaweza kutumika maeneo mbalimbali nchini na kusaidia kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu kwa vijana balehe.

Nae Prof. Al Zhao kutoka Chuo Kikuu cha Tsing Huan cha nchini China, amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na anaona unaenda kutatua changamoto ya upungufu wa damu kwa vijana balehe na bidhaa hizo ziko rafiki kwa watoto watakaohitaji kuzitumia.

Profesa Al Zhao kutoka Chuo Kikuu cha Tsing Hua (kushoto) akimkabidhi tuzo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Germana Leyna ikiwa ni ishara ya kutambua mchango unaotolewa na Taasisi katika utekelezaji wa afua mbalimbali za Kilishe.