TFNC YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI KUDHIBITI MAGONJWA YASIYO AMBUKIZA.

Imewekwa: 11th Jun, 2021
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari Wa mkoa wa Dar es salaam kwa ajili ya kuwapa elimu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha jambo ambalo litawasaidia kuelimisha jamii namna bora ya kuishi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa wanahabari hao, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Ray Masumo, amesema kuwa wanahabari ni wadau muhimu katika kuelimisha jamii ikiwemo kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Dkt. Masumo amesema kuwa lengo la semina ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili kuepuka jamii kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanasababishwa na ulaji usiofaa na mtindo isiyo bora wa maisha kwa kutumia vyakula venye chumvi nyingi, mafuta mengi au vinywaji vyenye sukari nyingi ambapo ni miongoni mwa viashiria hatarishi vya kupata magonjwa yasiyoambukiza” amesema Dkt. Masumo.
Amefafanua kuwa mtindo isiyo bora wa maisha ni kutofanya mazoezi, matumizi ya sigara na tumbaku pamoja na unywaji wa pombe ambavyo usababisha mtu kupata magonjwa yasiyoambukiza.
Ameeleza kuwa kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanywa hivi karibuni zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la watu wenye uzito uliozidi pamoja unene uliokithiri hivyo kuwaeka kwenye hatari ya kupata la magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani pamoja na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
“Magonjwa yana athari kubwa katika maendeleo ya taifa letu, lakini yanawezekana kuthibitiwa endapo tutasaidiana kuelimisha jamii kwa kuandika taarifa sahihi ili watu waweze kufata taratibu za ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha” amesema Dkt. Masumo.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya TFNC, Dkt. Esther Nkuba, amesema kumekuwa na taarifa mbalimbali katika mitandao ambazo sio sahihi na kusababisha kujenga hofu kwa wagonjwa.