Watoa huduma katika vituo vya afya Dodoma wapatiwa mafunzo ya mkoba wa siku 1000

News Image

Imewekwa: 5th Mar, 2019

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kupitia ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Madaktari Pamoja na Afrika (CUAMM) imetoa mafunzo ya mkoba wa siku 1000 kwa watoa huduma wa ngazi ya vituo vya afya mkoani Dodoma.

Fatuma Mwasora Afisa Lishe Mtafiti ambaye ni mmoja wa wawezeshaji amesema kwamba mafunzo yanatolewa kwa siku tano kuanzia tarehe 04/03/2019 hadi 08/03/2019 ambapo jumla ya watoa huduma 30 kutoka wilaya mbili za Chamwino na Kongwa watapatiwa mafunzo hayo.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya afya ili kuboresha huduma za uzazi, ulishaji wa watoto wachanga na wadogo pamoja na kuwapa virutubishi vya nyongeza, na kuweza kuwasimamia vizuri watoa huduma wa ngazi ya jamii (WAJA) kuhakikisha kila mlengwa anapate elimu ya lishe kupitia mkoba wa siki 1000” amesema Mwasora.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. James Kilogwe wakati wa ufunguzi amewataka watoa huduma kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi na kuleta matokeo chanya yanayokusudiwa na Serikali katika kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto.

Mkoba wa siku 1000 unaelezea umuhimu wa lishe bora kwa mtoto chini ya miaka miwili (kuanzia mimba inapotungwa hadi anapotimiza umri wa miaka miwili baada ya kuzaliwa). Katika kipindi hiki mtoto anahitaji virutubishi zaidi ili kuendana na kasi ya ukuaji wake kimwili na kiakili.

Tafiti zinathibitisha kwamba mtoto akipata utapiamlo katika kipindi hiki, athari zake hazirekebishiki na anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile kisukari, baadhi ya saratani, na matatizo ya moyo atakapokuwa mtu mzima.