Dkt. Vincent aagiza elimu ya ulaji unaofaa kuwafikia wananchi

News Image

Imewekwa: 28th Feb, 2019

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Vincent Assey ameiagiza kamati ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayohusiana na ulaji usiofaa kuendelea kutoa elimu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha kwa wananchi ili kujizuia na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya moyo, baadhi ya saratani na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa.

Dkt. Vincent ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao kazi cha kamati hiyo ya kitaifa kilichofanyika tarehe 28 februari 2019 katika ukumbi wa Taasisi ya Chakula na lishe Tanzania (TFNC).

“Watu wengi hawana uelewa juu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha, hivyo kuwapelekea kula kwa mazoea. Mama lishe na Baba lishe wanawapa wateja wao wali na ugali kwa wingi kuliko mbogamboga na matunda. Sasa tuone ni kwa namna gani tunawajengea uwezo na kuleta mabadiliko ya tabia katika jamii” amesema Dkt. Vincent.

Mwenyekiti wa kikao hicho Grace Moshi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema kuwa kamati inajukumu kubwa la kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na uelewa juu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili kila mmoja achukue hatua stahiki katika kujilinda dhidi ya magonjwa hayo.