Bodi Yatembelea Rasilimali za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania

News Image

Imewekwa: 4th Feb, 2019

Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) wamefanya ziara ya kutembelea rasilimali za Taasisi tarehe 30 Januari, 2019. Mali zilizotembelewa ni pamoja na Idara ya Sayansi ya Chakula iliyoko eneo la Mikocheni ambapo ipo maabara kuu ya Chakula na Lishe na karakana ya kutoa mafunzo ya usindikaji wa chakula. Pia Bodi ilitembelea na kujionea mitambo ya uchapishaji iliyopo makao makuu ya Taasisi kwenye Barabara ya Barack Obama pamoja na nyumba zinazomilikiwa na Taasisi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar-es-salaam ikiwemo Kurasini, Chang’ombe, Mburahati, Mikocheni na Kinondoni C. Aidha; Wajumbe wa Bodi walipata fursa ya kutembelea na kugagua viwanja vitatu vilivyopo Mbezi Beach.

Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joyce Kinabo alieleza kwamba lengo la ziara hiyo ni kuwawezesha wajumbe wa Bodi kuzitambua mali za Taasisi na kuona hali halisi na namna ya kuziboresha na kuzitumia katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi.

“Tumefanya ziara ya kukagua mali za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ili kujionea hali halisina kwa namna gani tunaweza kuziboresha ili zilete tija kwenye utoaji wa huduma za lishe nchini na katika kuongeza mapato ya Taasisi” alisema Profesa Kinabo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ambaye aliongoza ujumbe huu, Daktari Elifatio Towo alisema kuwa Menejimenti imefurahishwa na maamuzi ya wajumbe wa Bodi kutembelea mali hizo kwani inaonesha ni kwa namna gani Bodi ipo tayari kuisaidia Taasisi katika kuboresha huduma za lishe na pia kutumia rasilimali hizo kuwa chanzo cha mapato.

Aidha amesema kwamba Menejimenti ya Taasisi ipo tayari kuyapokea na kuyatekeleza maagizo yote yatakayotolewa na bodi kwa ajili ya kuboresha mali hizo.